Wednesday 20 April 2011

WATOTO 4 WAMEKUFA NA 3 WAMEJERUHIWA VIBAYA.

MSIBA WA WATOTO NI MSIBA WA TAIFA LA TANZANIA.


Sehemu ya ukuta ulioanguka na kusababisha vifo vya watoto wanne wa shule ya awali ya Nia iliyopo Kimara B mjini Dar es Salaam.Picha na Yusuf Badi

WATOTO 4 waliokuwa wakisoma katika Shule ya Chekechea ya NIA iliyopo Kimara B, Matosa, Kinondoni jijini Dar es Salaam wamekufa na wengine 3 kujeruhiwa vibaya baada ya kuangukiwa na ukuta.

Tukio hilo limetokea jana saa 6.30 mchana baada ya ukuta wa nyumba jirani na shule hiyo kuwaangukia watoto hao waliokuwa wakicheza kwenye bembea.

Jeshi la Polisi wilaya ya kipolisi Kimara liliwataja watoto waliokufa ambao miili yao imehifadhiwa katika Hospitali Teule ya Tumbi kuwa ni Gladness Shimwela (5), Devotha Living (5), Ludatrice Lawrence (3) na Isaack Ndosi (5).

Watoto waliojeruhiwa walitajwa kuwa ni Angela Jonas (5), Asumwene Uswege (5) na Lilian Dominick (3) ambao wote wamelazwa katika Hospitali ya Tumbi.

Taarifa kutoka jeshi la polisi zilisema, mmiliki wa ukuta huo Bw. Amani Mashika ambaye hakuwepo wakati ukuta huo unaanguka bado hajapatikana ili kueleza nini hasa chanzo cha ukuta huo kuanguka.

Aidha jitihada za mwandishi wa habari hizi kuupata uongozi wa shule hiyo inayomilikiwa na mke wa Profesa Philemon Sarungi, Bi. Jackline Sarungi hazikufanikiwa kwa kuwa walikuwa wakishughulikia kutoa huduma kwa majeruhi ili kuwawahisha hospitalini.
Salaam za Pole kwa wazazi wote zinatoka kwa watotoz.blogspot.com na watoto wote duniani.

Mungu pokea roho za watoto wote waliotangulia, haki yao ulishaibariki na uwape uponyaji wa haraka majeruhi.Amen
MASAU BWIRE wa MAJIRA.

No comments:

Post a Comment